THAMANI MIFUKO UTT AMIS YAONGEZEKA KWA TRILIONI 2.2

Na Moshi said 

Dar es salaam 

15 Nov.2024

Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2024, viashiria vya kiuchumi vinaonesha kwamba Kampuni ya UTT AMIS pamoja na Mifuko inayoisimamia imeendelea kuimarika na kufanya vizuri zaidi.

Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi Mtendaji wa UTT AMIS Simon Migangala akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa Wawekezaji wa Mfuko wa Umoja (Umoja Fund) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Thamani ya Mifuko hiyo ambayo ni Umoja Fund, Wekeza Maisha, Jikimu, Liquid Fund na Bond Fund imeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 1.5354 Juni 30, 2023 hadi Shilingi Trilioni 2.2382 Juni 30, 2024.


"Hili ni ongezeko la Shilingi Bilioni 702.8, sawa na asilimia 45.7 ikilinganishwa na ongezeko la shilingi bilioni 538.9, sawa na asilimia 54.0 kwa mwaka uliopita," amesema Migangala.

Migangala amebainisha kuwa ongezeko la ukubwa wa mifuko umetokana na faida iliyopatikana katika uwekezaji pamoja na ongezeko la la idadi ya wawekezaji 79,519, sawa na asilimia 32 waliojiunga katika mifuko kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na Wawekezaji 47,480, sawa na asilimia 24 waliojiunga mwaka wa fedha uliopita.

"Kama nilivyosema hapo awali, kwamba mifuko yote imetoa faida nzuri kwa wawekezaji wake. Faida kwa Mfuko wa Umoja ilikuwa asilimia 12.1," ameongeza Migangala.

Akizungumzia kuhusu matarajio ya mwaka wa Fedha 2024/2025, Migangala amesema kwa kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kampuni ya UTT AMIS ulioishia Juni, 30, 2024, umekuwa na mafanikio makubwa zaidi ya ilivyotarajiwa.

"Kwa mfano thamani ya mifuko ilikisiwa kukua kutoka shilingi bilioni 290.7 Juni 30, 2019 mpaka shilingi bilioni 485.9 kabla ya kurekebishwa na kuwa shilingi bilioni 1,007.9 Juni 30, 2024. Hata hivyo thamani halisi ya mifuko mpaka kufikia Juni 30, 2024 ilikuwa ni shilingi Trilioni 2.2 ambayo ni mara mbili ya kiwango kilichotarajiwa," ameeleza Migangala. 

Migangala amesema katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa Mpango mpya, UTT AMIS inatarajia kukamilisha uboreshaji wa mifumo kama msingi wa kukuza biashara yake. 

Amesema taasisi pia itaendelea kufanyika kazi vipaumbele, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma na kuibua bidhaa zingine kwa maslahi ya wawekezaji na kuwa UTT AMIS itaendelea kuboresha huduma za uendeshaji kuwa za kisasa zaidi na kuhakikisha kuwa wawekezaji wanapata faida nzuri zaidi kadri ya maendeleo ya soko la Mitaji.

Naye  Mwenyekiti wa Bodi ya UTT AMIS Prof. Faustine Kamuzora amesema kuwa kwa zaidi ya miaka 20 ya uwepo wa UTT AMIS  ni dhahiri kuwa fedha nyingi zimetengenezwa na kugawiwa kwa wawekezaji.

"Ni furaha iliyoje kwa wawekezaji wenzangu ambao wamejaribu kufanya uwekezaji tulivu (passive investiment) ambao hutufanya kutengeneza faida tukiwa tumelala au tukiendelea kutekeleza majukumu mengine ya kimaisha," amesema Prof. Kamuzora.

Amewapongeza wawekezaji kwa uamuzi wao wa busara, imani na kuwekeza katika mifuko mbalimbali ya uwekezaji wa pamoja ya inayosimamiwa na UTT AMIS.

Powered by Blogger.