WAZIRI KOMBO AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WATUMISHI WA OFISI YA MAMBO YA NJE - ZANZIBAR

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), pamoja na Naibu Mawaziri, Mhe. Cosato Chumi (Mb.), na Mhe. Dennis Londo (Mb.), wamekutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Zanzibar, kwa lengo la kufahamiana.
Kupitia kikao hicho kilichofanyika Agosti 09, 2024 pamoja na maelekezo mengine Mhe. Waziri alisisitiza juu ya watumishi kufanya kazi kwa tija na ushirikiano kama timu moja, kuwa na nidhamu na kuzingatia itifaki katika utekelezaji wa majukumu ili kuhakikisha malengo na matarajio ya Serikali yanafikiwa.

Aidha, Waziri Kombo ametoa maelekezo mahsusi kwa watendaji wote wa Wizara kuhusu kujumuisha na kushirikisha ipasavyo Ofisi hiyo ya ZNZ kwenye JPCs, mikutano na shughuli nyingine, kuanzia hatua za awali za maandalizi. Vilevile, alielekeza taarifa zinazoandaliwa au zinazotokana na mikutano hiyi zioneshe mapendekezo na nini kifanyike haswa katika eneo la Diplomasia ya Uchumi.


 Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Silima K. Haji alishukuru uongozi wa Wizara kwa ushirikiano hususan kwenye upande wa rasilimali watu. Alieleza kuwa hivi karibuni ofisi hiyo imepatiwa maafisa mambo ya nje, mtunza kumbukumbu, Afisa TEHAMA na Madereva kwani uwepo wao ni muhimu katika ufanisi wa kazi wa ofisi hiyo.

Aidha alimuahidi Mhe Waziri Kombo kuwa Ofisi yake itatekeleza maagizo hayo muhimu ambayo yanalenga kuboresha itendaji kazi wa Wizara na Serikali kwa ujumla.

Powered by Blogger.