EAC TUMIENI IDADI YA WATU MLIYONAYO KUKUZA UCHUMI NA TEKNOLIJIA YENU-MPANGO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki inaweza kutumia vema idadi kubwa ya watu iliyopo hususani vijana katika kujiletea maendeleo kama itawekeza zaidi katika Elimu na Afya ya watoto.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Elimu wa Kikanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Sherehe za Mwaka wa Elimu wa Umoja wa Afrika 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC). Amesema ongezeko la watu katika mataifa ya Afrika Mashariki inatoa ishara ya ulazima wa kuongeza rasilimali zaidi za kifedha ili kukidhi mahitaji ya elimu bora na afya bora.
Makamu wa Rais amesema mwenendo wa idadi ya watu Afrika Mashariki inaweza kuwa baraka kubwa kwa kuendelea kuwa na vijana na watu mahiri wa kujenga uchumi ikiwa rasilimali watu hiyo itatumika kikamilifu.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ambapo imelenga kufanya elimu ya lazima kutoka miaka saba iliyopo sasa hadi miaka kumi ifikapo mwaka 2027/2028.
Ametaja pia hatua za uboreshaji wa miundombinu ya elimu kama vile madarasa ya kujifunzia, nyumba za walimu, kuboresha mazingira ya ufundishaji kwa kuhakikisha kuna walimu wa kutosha na nyenzo za kufundishia kama vile kompyuta na vitabu. Amesema lengo la serikali ni kuongeza ubora wa elimu, kuongeza upatikanaji wake na kuhakikisha kuwa elimu inatosheleza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya haraka ya teknolojia.
Makamu wa Rais amewashukuru washirika wa Kimataifa wanaoiunga mkono Tanzania katika mageuzi ya sekta ya elimu na kuukaribisha mpango mpya wa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (PEERS) ambao utasaidia uratibu wa mifumo ya elimu katika kanda. Aidha amesema Tanzania ipo tayari kufanya kazi pamoja katika mpango kazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuendeleza malengo ya kielimu.
Makamu wa Rais amesema Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki katika nyanja zote ikiwemo elimu.
Mkutano huo unahudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mawaziri wa Elimu na wawakilishi kutoka nchi wanachama za Afrika Mashariki, Wadau wa Maendeleo, Mashirika ya Kimataifa pamoja na Wadau wa Sekta ya Elimu.
Post a Comment