MKANDARASI WA MRADI WA UMEME MALAGARASI MATATANI BAADA YA WAZIRI KUTORIDHISHWA NA KASI YA UJENZI
📌 *Meneja Mradi atakiwa kuondolewa mara moja eneo la mradi mpaka uchunguzi utakapokamilika.*
Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi amesema hajaridhishwa na mwenendo wa mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 49.5 katika maporomoko ya maji ya mto Malagarasi kutokana na kuchelewa kwa utekelezaji wa kazi pamoja na kushindwa kuendana na masharti ya mkataba kwani amekuwa akitoa visingizio badala ya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba.
Mhe. Ndejembi amebainisha hayo Mei 10, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa kuzalisha umeme megawati 49.5 katika maporomoko ya mto Malagarasi mkoani Kigoma.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi ameagiza meneja wa mradi huo upande wa mkandarasi kuondolewa mara moja kwa kuwa sehemu ya vikwazo vinavyochelewesha utekelezaji wa kazi huku akiagiza kufanyika kwa ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha za malipo ya awali zilizotolewa kwa mkandarasi ili kubaini fedha hizo zimefanya kazi gani na kama hazijaelekezwa katika miradi mingine.
"Mradi huu wa Megawati 49.5 una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Kigoma, Katavi, Kagera na maeneo ya jirani kwani utaongeza nguvu kwenye gridi ya Taifa na pia utaimarisha upatikanaji wa umeme wa nchini kwani Serikali inataka kuona umeme unapatikana hivyo haitakuwa tayari kuvumilia ucheleweshaji unaosababishwa na wakandarasi wasiozingatia wajibu wao.
Mhe. Ndejembi ametoa muda wa wiki mbili kwa TANESCO kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha za awali na taarifa kuwasilishwa kwa hatua zaidi.
Pia amempongeza Mkurugenzi wa TANESCO kwa juhudi za kufanya vikao na mkandarasi huyo huku akieleza kuwa atazungumza na Waziri wa Mambo ya Nje ili kufikisha wasiwasi wa Serikali kwa Balozi wa China kuhusu uwezo wa kampuni hiyo kutekeleza mradi huo.
kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange ameeleza kuwa mradi wa kufua umeme wa megawati 49.5 unatekelezwa na Kampuni ya Dangfang Electric International Corporation(DEC) kutoka China ambapo ujenzi wa mradi huo ulianza April 30, 2024 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 30, 2027 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 300 pindi utakapokamilika.
Amesema baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakipunguza viwango vya utekelezaji (specification) ili kupunguza gharama na kukidhi matakwa ya zabuni, jambo ambalo limechangia kuchelewa kwa kazi hivyo amesisitiza kuwa tayari wamepokea maelekezo ya Waziri na wanaenda kuyafanyia kazi kwa kuwa mradi huo upo nyuma kwa asilimia kadhaa.



Post a Comment