TANESCO YAPOKEA MAGARI MENGINE MAPYA 51

📌Ni katika jitihada za  kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepokea magari mapya 51 kati ya magari 100 yanayotarajiwa kuwasili ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, hatua inayolenga kuongeza kasi na ufanisi wa utoaji wa huduma bora kwa wateja katika maeneo mbalimbali nchini.


Akizungumza Februari 06, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Usafiri Makao Makuu, Bw. Thomas Gowele, amesema magari hayo aina ya ‘Toyota Land Cruiser Double Cabin’ yatakuwa na mchango mkubwa katika kuwafikishia wananchi huduma ya umeme kwa wakati, hususan katika maeneo ambayo awali hayakuwa rahisi kufikika kutokana na changamoto za kimazingira.

“Tayari tumepokea jumla ya magari 51 kati ya magari 100 tunayotarajia kuyapata hivi karibuni. Tunaamini ujio wa magari haya utaongeza ufanisi na kasi ya kuwahudumia wateja wetu, hasa katika maeneo ya vijijini,” alifafanua Bw. Gowele.

Ametoa rai kwa watumishi watakaokabidhiwa magari hayo kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kutimiza dhamira ya Shirika ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya umeme ya uhakika.

TANESCO imeendelea kufanya jitihada za kununua vitendea kazi vya usafiri, yakiwemo magari madogo, malori bajaji na pikipiki, ili kuhakikisha maeneo yote yanayohitaji huduma ya umeme yanafikiwa kwa urahisi na ufanisi zaidi.
 

Powered by Blogger.