VIONGOZI WA SIASA,DINI, WANAHABARI HUBIRINI AMANI KWA TAIFA:DKT MWINYI
Ameeleza kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo katika nchi yoyote inayotaka ustawi na maendeleo ya wananchi wake.
Alhaj. Dkt. Mwinyi amesema si sahihi kwa wanasiasa na viongozi wa vyama kuwasisitiza wapiga kura kulinda kura baada ya kupiga kura, kwani jukumu hilo kwa mujibu wa sheria hufanywa na mawakala wa uchaguzi na si vinginevyo.
Amebainisha kuwa hatua ya kuwataka wananchi kulinda kura inaweza kuchochea uvunjifu wa amani, jambo lisilostahiki katika kipindi hiki ambapo nchi imedumu katika hali ya amani, maelewano na utulivu mkubwa.
Aidha, amesema kuwa bado Zanzibar inahitaji maendeleo zaidi, hivyo kudumisha amani ni jambo la lazima ili Serikali iendelee kutekeleza mipango yake ya maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipojumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa na Dua maalum ya kumuombea pamoja na kuliombea Taifa, iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Al-Abrar, Tazari, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amewanasihi waumini wa dini ya Kiislamu kuyazingatia mafunzo na maelekezo ya Mtume Muhammad (SAW) ili kuepukana na shari na uvunjifu wa amani.
Naye Khatibu wa msikiti huo, Sheikh Omar, amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa maendeleo makubwa aliyoyatekeleza kwa wananchi wa Tazari na Mkoa wa Kaskazini kwa ujumla katika huduma za elimu, afya na miundombinu ya barabara, na ameahidi kuendelea kumuombea mafanikio zaidi.
Post a Comment