TANZANIA BLOGGERS NETWORK YAINGIA MCT RASMI

Mwenyekiti Asema Uanachama ni Njia ya Kulinda Weledi na Uhuru

Na Mwandishi wetu

Tanzania Bloggers Network (TBN) imepiga hatua kubwa katika kutambulika rasmi baada ya kukabidhiwa hati za uanachama katika Mkutano Mkuu wa 27 wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), uliofanyika Septemba 25, 2025, jijini Dar es Salaam. TBN ilikuwa miongoni mwa wanachama wapya wanane (8) waliojiunga na Baraza.

Akizungumza baada ya makabidhiano, Mwenyekiti wa TBN, Ndugu Beda Msimbe, alisema kuna manufaa makubwa kwa wanablogu kujiunga na MCT.

"Uanachama huu unatoa uhalali na kutambuliwa rasmi kwa wanablogu mbele ya jamii, Serikali na wadau wengine. Tunajumuishwa katika familia kubwa ya vyombo vya habari vinavyojisimamia, na sasa wanablogu wanatambulika kama chanzo cha habari kinachowajibika," alisema Ndugu Msimbe.

Aliongeza kuwa, TBN sasa inafaidika na mfumo wa ulinzi wa Baraza, hasa katika masuala ya usuluhishi dhidi ya malalamiko. Alisisitiza kuwa mfumo huo utawalinda wanablogu kisheria na kiuchumi dhidi ya vitisho au uwezekano wa kufilisiwa kutokana na faini za kimahakama, kwa kuwa sasa wana kimbilio katika Kamati ya Maadili ya MCT.

Upanuzi huu unakwenda sambamba na wito uliotolewa na uongozi wa MCT unaosisitiza umuhimu wa mshikamano wa wanachama.

Katibu Mtendaji wa MCT, Bw. Ernest Sungura, alikumbusha kwamba kauli mbiu ya mkutano, “Uhai wa Wanachama ni Nguvu na Usalama wa Taaluma ya Habari,” inapaswa kuwa mwongozo.

"Ikumbukwe ni wanachama waliosema siku moja tujisimamie au lah tukubali kufa... Uhai wa wanachama upo katika kushiriki vikao na kulipa ada za uanachama," alisema Bw. Sungura, akionya kuwa enzi za kudhani wafadhili watatoa fedha kwa MCT zimekwisha, na hivyo uhai wa Baraza unategemea wanachama.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Ndugu Yusuf Khamis Yusuf, alisisitiza kuwa katika miaka hii 30 ya MCT tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995, Baraza limejipambanua kama taasisi huru inayolinda weledi na maadili.

Weledi na Uhuru: Njia ya Baraka

Akifungua rasmi Mkutano huo, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, Rais Mstaafu wa Nne wa Baraza, alisisitiza kuwa uwepo wa MCT umeokoa vyombo vingi vya habari kutokana na kufilisiwa.

Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila chombo cha habari, ikiwemo TBN, kuwa kiungo cha ukweli bila kuegemea upande mmoja. Alitahadharisha wanahabari akisema: "Kusimama kwenye haki ni kugumu kuliko kujipendekeza. Kusimama na haki kunahitaji sadaka. Siyo njia nyepesi au rahisi, lakini ni njia ya baraka mno na ni njia inayompendeza Mungu."

Jaji Mihayo pia alizindua rasmi Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT 2025) ambazo zitaendeshwa kwa mfumo wa kidijitali sambamba na tovuti mpya ya MCT, hatua inayodhihirisha dhamira ya Baraza kukuza weledi katika tasnia nzima.

 

Powered by Blogger.