STERGOMENA TAX AZINDUA BODI MPYA YA WAKURUGENZI SHIRIKA LA MZINGA


Na Mwandishi wetu 

20.08.2025

Morogoro

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena  Tax , tarehe 20 Agosti, 2025, mkoani Morogoro amezindua Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Mzinga,itakayoongozwa na Luteni Jenerali Mstaafu Balozi, Charles Makakala, aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan.
Akizindua Bodi hiyo ya 18 ya shirika hilo,Waziri wa Ulinzi Tax amewapongeza wajumbe hao wapya wa bodi hiyo ya shirika la Mzinga kwa kuteuliwa kwao kuliongoza Shirika la Mzinga na akawaambia ni imani ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naye pia kuwa Shirika litapiga hatua kubwa zaidi katika kukidhi madhumuni ya kuanzishwa kwake Septemba 1974.

Waziri Tax amewaambia Wajumbe hao wapya wa Shirika la Mzinga kuwa hadi sasa shirika hilo limepiga hatua kubwa na nzuri katika miaka ya karibuni ambapo kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mazao ya Msingi umeongezeka na Shirika limekuwa na miradi mingi yenye tija kwa Taifa na kuleta maendeleo. Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Tax ameitaja miradi hiyo kuwa ni Ukarabati wa miundombinu ya shirika, makazi ya watumishi na kuwekeza katika Hospitali ya Mzinga na hivyo kupekelekea kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya rufaa ya Mkoa kuanzia tarehe 02 Agosti 2025.
Waziri wa Ulinzi na JKT akatoa Pongezi zake za dhati kwa Meneja Mkuu wa Mzinga, Brigedia Jenerali Seif Hamisi  na timu yake pamoja na bodi iliyomaliza muda wake kwa kujituma,ubunifu na kazi nzuri iliyoleta mafanikio hayo aliyoyataja.
Aidha, Waziri wa Ulinzi na JKT, ametoa rai kwa bodi mpya aliyoizundua kushirikiana na menejimenti kuyaendeleza mafanikio hayo, na pia akawataka kuongeza  jitihada ili uzalishaji  na utendaji uimarike zaidi. Waziri Tax akawaambia, “tuongeza juhudi za uwekezaji katika hospitali yetu ambayo ni tegemeo kubwa si kwa wana Mzingo pekee, bali pia kwa Mkoa wa Morogoro na Taifa, ili kuendana na mahitajio ya sasa na siku za usoni”.
Waziri wa Ulinzi Tax akawakumbusha Bodi mpya ya Mzinga jukumu jipya la Kitaifa lililopewa Shirika la Mzinga la kuzalisha zao la msingi kwa ajili ya nchi ya Angola. “Kazi hii ikikamilika kwa ufanisi na kwa wakati italiletea heshima Shirika letu. Kwa ajili hiyo, tuweke mikakati madhubuti ili kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi na kwa wakati.  

Aidha, ni wajibu wenu kuhakikisha kwamba taarifa za mipango yenu ya maendeleo zinakuwa shirikishi ili wadau wote wanaohusika waweze kutoa ushirikiano kwa nafasi zao”.
Tukio la Uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Mzinga iliyozinduliwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilihudhuriwa pia na Wageni mbalimbali toka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Viongozi vyama vya Wafanyakazi, Wawakilishi toka Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wawakilishi  wa wavumbuzi na wabunifu wa shirika hilo.




Powered by Blogger.