RC CHALAMILA AZINDUA MKAKATI WA VIKAO KAZI KATI YA TANESCO NA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe.Albert Chalamila amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kulinda miundombinu ya umeme katika maeneo wanayoyaongoza ili kuzuia hasara kwa Serikali inayotoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na wananchi.

Mhe.Chalamila ameyasema hayo leo Juni 24, 2025 wakati akizindua kikao kazi kati ya TANESCO na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ubungo ambapo amewataka Wenyeviti hao kushirikiana na Wananchi kulinda mindombinu hiyo na kuwa tayari kusikiliza kero zinazowakabili hasa zinazohusu masuala ya umeme.

“Transfoma ikiibiwa umeme ukakosekana mtaa wako. Kiwanda kilichoajiri wananchi kikashindwa kuzalisha, amani itatoweka. Hii ni kwa sababu wafanyakazi hao watashindwa kulipwa kutokana na kutokuwa na uzalishaji. Ndio maana Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO ameona awaite hapa ili mkimuona mtu anaiba Transfoma wajue madhara yake kwa wananchi wanaowaongoza,” amesema Mhe. Chalamila.

Aidha amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange kwa kikao kazi hicho huku akiwaasa viongozi hao kuipa ushirikiano menejimenti ya TANESCO katika mitaa wanayoiongoza ili kufanikisha azma ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika.

“Nawapongeza sana TANESCO kwa kuandaa kikao kazi hiki. Dar es Salaam ni sehemu muhimu ulipo uzalishaji mkubwa wa umeme. Kwa hatua hii ya kuwakutanisha viongozi hawa wa Serikali za Mitaa ni fursa nzuri kwa kuwa wanakutana moja kwa moja na wananchi hivyo ni rahisi kuwabaini hata wale wenye nia ovu ya kuharibu miundombinu ya umeme,’’alisisitiza Mhe.Chalamila.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Twange amesema licha ya kufanya kazi kubwa ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme bado Shirika limejizatiti kuhakikisha huduma bora inawafikia wateja kwa haraka na kwa wakati sahihi, akisisitiza mkutano huo pia umelenga kuwa karibu na wananchi kupitia Wenyeviti hao wa Serikali za Mitaa.

‘’TANESCO tumejitahidi kuwa karibu na wananchi kupitia kituo chetu cha huduma kwa wateja, tunamshukuru sana Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Miradi inakamilika na wananchi wanapata umeme wa uhakika. Kazi  yetu ni kuendelea kupanga mikakati ya kuhakikisha wananchi wanaunganishiwa umeme  na kupata huduma bora,’’ liafafanua Bw.Twange.

Hata hivyo, miongoni mwa matukio mengi, Bw Twange, ametumia sehemu ya Mkutano huo kutoa zawadi ya majiko yanayotumia umeme Kidogo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe.Albert Chalamila na baadhi ya Wawakilishi wa Serikali za Mtaa kwa lengo la kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme ikiwa ni ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Powered by Blogger.