BOLT YAREKODI UPUNGUFU WA ASILIMIA 51 YA SAFARI ZA NJE YA NCHI MFUMO TANZANIA


 Dar es Salaam, Tanzania

Kampuni ya usafiri wa mtandaoni ya Bolt Tanzania imetangaza kupungua kwa asilimia 51 ya safari zinazofanyika nje ya mfumo wa app (offline trips) katika kipindi cha miezi sita iliyopita. Hii inafuatia utekelezaji wa hatua madhubuti za kiusalama zilizolenga kulinda usalama wa abiria na madereva, na kuimarisha uwajibikaji katika sekta ya usafiri wa kisasa.


Kampuni imetaja kushuka kwa safari hizo kama matokeo ya udhibiti mkali, ikiwa ni pamoja na utambuzi wa mapema wa mienendo isiyofuata taratibu na utekelezaji wa hatua kali dhidi ya safari zisizofuata mfumo. 

Safari za nje ya app huzuia matumizi ya vipengele vya usalama kama ufuatiliaji wa GPS, utambulisho wa abiria na dereva, pamoja na msaada wa dharura.

“Kupungua kwa safari za nje ya mfumo ni dalili kuwa soko linaelekea kwenye mwelekeo wa usafiri wa kuaminika na salama zaidi,” alisema Dimmy.

 Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt Tanzania na Kenya.

 “Ni ushahidi wa kazi yetu ya ndani kuhakikisha kuwa kila safari inayoendeshwa kupitia Bolt inalindwa na kufanyika kwa uwazi.”

Bolt imeanzisha mikakati mbalimbali kusimamia mabadiliko haya, ikiwemo sera ya kutovumilia kabisa safari za nje ya mfumo, mfumo wa ufuatiliaji wa safari kwa wakati halisi, na teknolojia ya kuchambua na kutambua mienendo ya kutiliwa shaka.

Wakati safari za nje ya mfumo bado ni changamoto katika sekta nzima ya usafiri wa mtandaoni, hasa kutokana na hatari zinazotokana na kutofuatiliwa au kutothibitishwa kwa safari hizo, Bolt inaendelea kuonesha dhamira ya kujenga mfumo salama wa usafiri wa kuaminika hapa Tanzania.

“Usalama si kipengele tu cha app, ni utamaduni tunaojenga safari baada ya safari,” aliongeza Kanyankole.

 “Ingawa tuna sababu ya kujivunia hatua hii, bado tuna safari ndefu. Tutashirikiana kwa karibu na wadau wa sekta, wasimamizi wa sheria, na umma kwa ujumla ili kuinua viwango vya usalama.”

Bolt inaendelea kuwasihi abiria kutumia app pekee kufanya miamala ya safari, na kuepuka kukubali safari za mtaani hata kama zitaombwa na madereva. Kutumia app kunawapa abiria huduma muhimu kama ufuatiliaji wa safari kwa wakati halisi, tathmini za madereva, arifa za dharura (SOS) na msaada wa wateja masaa 24 kila siku.

Kampuni pia imesisitiza nia yake ya kuendelea kuwekeza katika teknolojia na ushirikiano unaolenga kuimarisha usalama na uwajibikaji katika sekta ya usafiri wa mtandaoni.

Powered by Blogger.