BODI YA ITHIBATI (JAB) YAANZA KUSAJILI WAANDISHI KIDIGITI
19.05.2025
Hatimaye Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Tido Mhando amesema Waandishi wa habari watakaobainika wamewasilisha vyeti au nyaraka za kughushi katika ujazaji wa vitambulisho kwa njia ya mtandao, watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Hatua hizo zitajumuisha kufutiwa mara moja usajili wao, ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki,
Pia kupigwa marufuku kujihusisha na shughuli za uandishi wa habari au majukwaa mengine ya kitaaluma.
Mhando amesema hayo leo Mei 19, 2025 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu uzinduzi rasmi wa maombi ya Ithibati na vitambulisho vya wana habari vijulikanavyo kama Press Card.
Amesema, “Bodi imekaa vizuri hatutapenda tuchezewe katika hilo. Mtu akisema anafanya najaribio, akaingia katika hali ambayo inamhuzunisha asituhukumu. Sisi tutafuata vigezo vinavyoeleweka,”.
Ameonya tabia ya vyuo vinavyojiandaa kutoa au tayari vimetoa vyeti vya kughushi visijaribu kufanya hivyo kwa kuwa lengo la JAB ni kuipa heshima fani ya habari.
“Wakati umefika wa kuheshimisha tasnia yet. Tunataka watu watuheshimu kama tasnia nyingine zinavyoheshimika.
“Kumekuwa na taarifa zinazodokeza kuwepo kwa baadhi ya watu wanaojaribu kuwasilisha vyeti vya kughushi au nyaraka zisizo halali kwa lengo la kujipatia usajili na vitambulisho kinyume na taratibu.
Tunapenda kusisitiza kuwa jambo hilo si tu linakiuka maadili ya taaluma ya habari, bali pia ni makosa ya jinai yanayoadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi,” amesema.
Amewakumbusha wana habari kuwa,
Mfumo wa TAI HABARI umeanzishwa kwa nia njema ya kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari kwa misingi ya uwajibikaji, weledi na heshima.
Amesema lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwandishi aliyesajiliwa ni mtu mwenye sifa stahiki, mafunzo sahihi, na anayezingatia maadili ya kazi hiyo muhimu kwa jamii.
Post a Comment