SERIKALI YAOMBWA KUWAJALI WAWEKEZAJI WAZAWA
Na Moshi saidi
Dar es salaam
Serikali imeombwa kuwakumbuka na kuwajali wawekezaji wa ndani kwa kuwapa ruzuku ili kuweza kuwaongezea thamani wazawa katika kukuza uchumi wa nchi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya Utege technical service Interprises Ltd, OTIENO IGOGO ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya chuo cha Ushirika Vocational Training Center jijini Dar es salaam.
Igogo ameiomba serikali kuendelea kuwatia moyo wawekezaji wa ndani ili kuweza kukuza masoko na mitaji yao kulingana na uwekezaji wanaoufanya.Aidha amewataka wahitimu hao kutokaa Vijiweni na kulalamika badala yake wajiunge kwenye vikundi vilivyo rasmi na kusajiliwa ili kuweza kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri katika kujikwamua na lindi la umaskini.
Katika hatua nyingine mgeni huyo rasmi katika mahafali ya chuo hicho cha Ushirika amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa kiuzalendo katika kuwajali na kuwathamini wananchi kwa kuridhia kutolewa tena kwa mikopo hiyo ya Halmashauri hapa nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa chuo hicho Magoye Machela ameisihi Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kukiunga mkono chuo hicho cha Ushirika katika kukisaidia ili kiweze kuendana na soko la ajira kulingana na elimu inayotolewa chuoni hapo.
Machela amesema wao kama chuo wanamuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika suala zima la elimu bure kutokana na chuo hicho kuzalisha wanafunzi wengi walio na elimu ya kawaida inayopelekea kuajiriwa katika maeneo mbalimbali kulingana na fani walizosomea kupitia chuo hicho.
Nao baadhi ya wahitimu wa chuo hawakusita kuelezea furaha yao baada ya kuhitimisha masomo yao.
Hayo ni mahafali ya 7 yaliyofanyika chuoni hapo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022.
Post a Comment