TANESCO YATAKIWA KUBUNI TEKNOLOJIA MPYA KUBORESHA HUDUMA KWA WATEJA
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ameielekeza TANESCO kuendelea kufanya tafiti na kubuni teknolojia mpya zitakazorahisisha utoaji wa huduma kwa wateja nchini.
Amesema dunia inabadilika kwa kasi kubwa hivyo Shirika hilo linapaswa kuendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuongeza ufanisi na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa urahisi.
Akifungua mkutano wa mwaka wa Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO unaofanyika mkoani Dodoma, Mhe. Salome amesema matumizi makubwa ya mifumo ya kidijitali pamoja na akili mnemba yatasaidia kuboresha mawasiliano na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi wanapohitaji huduma za umeme.
Aidha, ameagiza kufanyika kwa maboresho katika manunuzi ya vifaa pamoja na kuongeza uwezo wa vituo vya huduma kwa wateja ili kupunguza ucheleweshaji wa huduma.
Amesema hatua hizo zitasaidia kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuweka tabasamu kwa wananchi wanaotegemea huduma za TANESCO kila siku.Mhe. Salome pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya idara mbalimbali ndani ya Shirika ikiwemo TEHAMA, usambazaji na huduma kwa wateja. Amesema huduma bora hutokana na ushiikiano mzuri wa watumishi wote katika kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa kwa wakati.






Post a Comment