WANUFAIKA WA MITAJI YA COOKFUND WAHIMIZWA KUWEKEZA KATIKA MITUNGI MIDOGO YA GESI
📌 *Lengo ni kuwezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu gharama*
📌 *Wasisitizwa matumizi ya Mita janja (smart meters) ili kuwezesha wananchi kununua gesi kama LUKU.*
Mkurugenzi wa Nishati safi ya Kupikia Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay ameyasema hayo wakati akiendelea na ziara yake jijini Mwanza kwa lengo la kukagua miradi ya Nishati Safi ya Kupikia inayofadhiliwa na Cookfund
ambayo inalenga kuchochea maendeleo ya nishati safi ya kupikia nchini.
Akiwa jijini Mwanza Mlay aliwatembelea wafanyabiashara wa kuuza gesi walioongezewa mtaji kupitia mradi huo wa CookFund ili kuhakikisha Wananchi wanafikiwa na huduma ya gesi kwa ukaribu zaidi kupitia uinuaji wa wafanyabiashara wadogo na wa kati kwenye sekta ya nishati safi ya kupikia.
Amesema kupitia Cookfund wafanyabiashara wadogo wanapewa mitaji na msaada wa kiufundi ili kuongeza wigo wa usambazaji wa majiko bora ya gesi na mitungi ya gesi.
Mlay amewapongeza wanufaika hao wanaouza mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku kwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma hiyo kwa wakati na urahisi zaidi huku akizidi kusisitiza kuhusu kuuza pia mitungi ya gesi ya kilo moja hadi tatu.“Tunahitaji kuona wanufaika wa CookFund wakiwekeza kwenye teknolojia zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Mitungi midogo ni suluhisho linalowezesha watu wengi zaidi kutumia gesi badala ya kuni au mkaa”. Amesema Mlay
Sambamba na hilo, Mlay ametoa wito kwa wadau wote wa nishati safi ya kupikia kuleta teknolojia ya mita janja (smart meter) kwa baadhi ya maeneo ambayo bado hawana ili kurahisisha ununuzi wa gesi kwa njia ya kidigitali, na kuondoa changamoto za kujaza mitungi kwa gharama kubwa au umbali mrefu.
Vilevile amewataka wananchi kuendelea kuchukua hatua za kubadilika na kutumia nishati safi za kupikia ikiwemo gesi, umeme, mkaa mbadala na bayogesi kwa ajili ya afya bora na mazingira salama.
Kwa upande wao, Wafanyabiashara wanaouza mitungi ya gesi wamesema kuwa mwitikio kutoka kwa wananchi umekuwa mkubwa huku baadhi ya wananchi wakikopeshwa mitungi na wengine wakijitokeza kuwekeza kwa kulipa fedha kidogokidogo ili kuweza kupata mitungi hiyo ya gesi ili kuachana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa afya na mazingira.
Post a Comment