TRC NA TAA ZAINGIA MAKUBALIANO KUUNGANISHA MIUNDOMBINU PANDE MBILI

Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) zimetia saini hati ya makubaliano ya kuunganisha miundombinu ya reli na viwanja vya ndege kwaajili ya kuongeza ufanisi na kuwarahisishia abiria kuingia na kutoka katika viwanja vya ndege nchini.

Makubaliano hayo yamesainiwa kwa niaba ya taasisi mbili hizo na  Mkurugenzi Mkuu wa TRC Mha. Machibya Shiwa na Mkurugenzi Mkuu TAA Bwa. Abdul Mombokaleo,  katika ukumbi wa mikutano TAA jijini Dar es Salaam Septemba 26, 2025.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TRC Mhandisi Machibya Shiwa,  amesema kuwa katika makubaliano hayo TRC  watakuwa na jukumu la kujenga miundombinu ikiwemo njia ya reli na vituo vya treni ili kuleta muunganiko kati ya reli na viwanja vya ndege

TRC tumeshakamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mtandao wa reli katika jiji la Dar es Salaam aidha  kiwanja hiki cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyere (JNIA) kimeunganishwa na reli hiyo na  kwa upande wa Dodoma pia tumekamilisha upembuzi kwaajili ya kuunganisha Stesheni ya Dodoma na kiwanja cha ndege cha Msalato” alisema Mkurugenzi Mkuu huyo wa TRC.

Mha. Shiwa alisisitiza kuwa “jambo hili ni maelekezo ya Mhe. Rais aliyoyatoa Julai 31, 2025  wakati wa uzinduzi wa treni za mizigo Kwala na alipokuwa anazindua safari za treni za abiria mwaka 2024 ambapo alielekeza TRC tushirikiane na TAA kujenga tawi la reli linaloingia Julius Nyerere International Airport” amekumbusha Mha. Shiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TAA amesema kuwa ukuaji wa miundombinu pamoja na kurahisisha maisha ya watu,  unasaidia pia katika  kukuza uchumi, na kukuza pato la Taifa, hivyo makubaliano hayo yanalenga kuboresha huduma ya usafiri kati ya anga na reli lakini pia kuleta faida zitakazopatikana katika maeneo kutokana na uwepo wa mradi huu.

Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania inaendelea na uboreshaji na ujenzi wa miundombinu mipya reli ya kisasa (SGR) nchini ili kuongeza ufanisi katika sekta ya uchukuzi na kuleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
 

Powered by Blogger.