MHANDISI MRAMBA NA JICA WAJADILI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA NISHATI
📌 *Awasisitiza JICA kuwajengea uwezo wataalam wazawa katika usanifu wa mitandao ya usambazaji Gesi Asilia*
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amekutana na Wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ili kujadili hali ya utekelezaji wa miradi ya Nishati inayofadhiliwa na shirika hilo kwa lengo la kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Miradi iliyojadiliwa kwa kina katika kikao hicho ni wa kusafirisha umeme kutoka Tanzania hadi Uganda (UTIP) na mradi wa umeme Dodoma Ring Circuit unaolenga kuzidi kuimarisha hali ya upatikanaji umeme Dodoma.
Katika kikao hicho, Mha. Mramba ameisisitiza JICA kuhusu suala la utekelezaji mradi wa mfano wa usambazaji gesi asilia katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambao utakuwa kielelezo cha manufaa ya gesi asilia iliyogunduliwa hapa nchini ambayo itasaidia pia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Vilevile, Mramba ameishukuru JICA kwa kufadhili miradi ya Nishati ambayo imekuwa chachu ya maendeleo nchini hususan katika Jiji la Dodoma ambalo linaendelea kukua kwa kasi.
Post a Comment