UTEUZI WA SAMIA ULIFUATA TARATIBU NA KANUNI ZOTE: KIKWETE
Na Mwandishi wetu
28.08.2025
Dar es salaam
Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Jakaya Kikwete amesema mchakato wa kumteua mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan ulifuata utaratibu wa siku zote, na kwamba kwa wale walioona mchakato huo haukufuata taratibu hawafahamu taratibu za chama hicho.
Dkt. Kikwete amesema hayo wakati akitoa salamu katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi za CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, unaofanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.
Amesema anashangaa kuona watu wanabeza uteuzi huo wakati wengine walishiriki katika michakato ya teuzi za wagombea wa awamu zilizopita ambao unafanana na mchakato uliofuatwa kwa awamu hii.
Dkt. Kikwete ametumia jukwaa hilo kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza kwa kishindo miradi mbalimbali iliyoachwa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Magufuli, ambapo pia ametekeleza ilani ya CCM kwa kishindo kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika kila sekta.
Dkt. Kikwete pia amesema Dkt. Samia amekamilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, huku akimuita ni kiongozi mwenye maono ya mbali.
Post a Comment