SERIKALI YA TANZANIA YAENDELEA KUTHAMINI MCHANGO WA MAJENERALI WASTAAFU KWA TANZANIA YAWAKABIDHI MAGARI MAPYA YA KISASA

Na Mwandishi wetu 

15.07.2025

Dar es salaam 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) tarehe 15 Julai, 2025 katika Ofisi ndogo za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga amewakabidhi Magari Mapya ya Kisasa Maafisa Jenerali watano wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ikiwa ni katika kutambua utumishi wao uliotukuka katika nchi ya Tanzania.

Akiongea muda mfupi kabla ya kumkabidhi magari hayo aina ya Toyota Prado toleo jipya la mwaka 2025 Mhe. Waziri Tax amesema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa Majenerali hao na Majenerali wengine waliostaafu kwa taifa la Tanzania, ambapo amesema pamoja na kwamba hii ni stahiki yao, lakini stahiki hiyo inatokana na kutambua mchango wa majenerali wastaafu katika Ulinzi wa Taifa letu, lakini kipekee mchango wao katika vipindi mbalimbali vya utumishi wao wa kiadilifu na heshima ambapo vimeendelea kulifanya Taifa la Tanzania kuwa imara.

Waziri Tax amewaambia Majenerali hao Wastaafu kuwa “Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan analithamini sana Jeshi lake, anawathamini sana nyinyi waanzilishi, anawathamini sana wote waliochangia katika kuimarisha Ulinzi wa Taifa letu kuhakikisha mipaka ipo salama, hivyo kwa kulitambua hilo amewawezesha.

Majenerali wote waliokuwa wamefikia muda wa kubadilishiwa magari wabadilishiwe, naomba niwakabidhi magari haya yaendelee kuwasaidia na kuwapa faraja katika maisha yenu, pamoja na kwamba mmestaafu bado ni hazina na muendelee kutusaidia na kutushauri” alisema Mhe. Waziri wa Ulinzi na JKT.

Kukabidhiwa magari hayo majenerali wastaafu wa JWTZ  ni stahiki ya Majenerali Wastaafu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya  ya mwaka 1966 pamoja na kanuni zake  za mwaka 2015 ambazo zinasema Jenerali wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania baada ya kustaafu atakabidhiwa Gari Jipya la wakati husika
Naye Luteni Jenerali Mstaafu, Balozi Wnyjones Mathew Kisamba, akiongea kwa niaba ya majenerali wastaafu waliokabidhiwa Magari hayo mapya, amemuomba Waziri wa Ulinzi na JKT kuwafikishia Shukrani zao za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu na serikali yake kwa kuendelea kuwakumbuka wastaafu na kuwajali, na pia amemshukuru Waziri wa Ulinzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi kwa kuwa nguzo  imara kwao Wastaafu.







 

Powered by Blogger.