WAGENI ZAIDI YA 500 DUNIANI KUSHUHUDIA TUZO ZA 32 ZA UTALII KANDA YA AFRICA,DAR ES SALAAM
Na Jumanne Magazi
11.06.2025
Dar es salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Balozi Ephraim Mafuru amewataka wadau wa utalii nchini kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta hiyo ikiwemo usafirishaji, huduma za afya, burudani na malazi ili kukuza utalii na kuongeza vipato vyao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mafuru alisema kuwa sekta ya utalii ina nafasi kubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi endapo wadau wataitumia kikamilifu.
Balozi Mafuru alikuwa akizungumzia maandalizi ya Tuzo za 32 za Utalii wa Kimataifa kwa ukanda wa Afrika na Bahari ya Hindi, zinazotarajiwa kufanyika Juni 28 mwaka huu, tukio ambalo linatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Naye Meneja wa Hoteli ya Johari Rotana, Ahmed Said, alieleza kuwa ujio wa wageni kutoka mataifa mbalimbali kupitia tuzo hizo ni fursa adhimu kwa sekta ya hoteli kuonyesha ukarimu wa Kitanzania pamoja na kuitangaza Dar es Salaam na vivutio vyake kama sehemu ya kipekee kwa wageni wanaokuja kwa mapumziko au shughuli za kikazi.
Kwa ujumla, maandalizi ya tuzo hizo yameibua hamasa miongoni mwa wadau wa utalii, huku matarajio yakiwa ni kuinua hadhi ya Tanzania kimataifa kupitia utoaji wa huduma bora na vivutio vyake vya kipekee. Wadau wanaamini kuwa kupitia matukio ya aina hii, Tanzania itazidi kujiimarisha kama kitovu cha utalii barani Afrika.
Post a Comment