AIRTEL TANZANIA NA NEMC WAONGOZA USAFI MBEZI BEACH KIDIMBWI KUPAMBANA NA TAKA ZA PLASTIKI


 Kampuni ya simu ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), wamefanya zoezi la usafi katika fukwe za Mbezi Beach Kidimbwi huku wakitoa msaada wa vifaa vya usafi kwa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach B, kupitia kampeni yao ya “Pamoja Tutokomeze Taka za Plastiki.”

Katika zoezi hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Kudhibiti Airtel, Bi. Beatrice Singano, alisema Airtel imejipanga kuhakikisha kampeni hiyo inakuwa endelevu kama sehemu ya kuunga mkono Ajenda ya Taifa na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda na kutunza mazingira.

“Katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu ndipo kuna taka nyingi hasa taka ngumu zisizooza kama plastiki na chupa. Wakati wa zoezi hili tumeshuhudia wingi wa taka hizo. Niiombe jamii itunze mazingira kwa kuzitenga na kuzitupa taka katika sehemu sahihi kwa ajili ya uchakataji,” alisema Bi. Singano.

Sambamba na zoezi hilo, Airtel pia ilikabidhi vifaa vya kufanyia usafi kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach B, vitakavyosaidia kuendeleza utunzaji wa mazingira katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki, Jeremia Nyakwaka, alisema wamefanya usafi wa kina katika fukwe hizo na kukuta taka nyingi zikiwa ni plastiki na chupa, zinazosababishwa na utupaji hovyo wa taka ambao huishia baharini na mito.

“Natoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kuepuka kutupa taka hovyo, hasa plastiki na chupa ambazo ni hatari kwa afya na mazalia ya viumbe hai,” alisisitiza Nyakwaka.

Aidha, aliishukuru Airtel Tanzania na wananchi waliotoa ushirikiano katika zoezi hilo na kusisitiza kuwa NEMC ipo tayari kushirikiana na wadau wote wanaojali mazingira.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach B, Bi. Asha Vionatis, alisema kuwa kipaumbele chao ni utunzaji wa mazingira na kwamba ushirikiano wa aina hii unasaidia sana juhudi wanazozifanya kama mtaa.

“Tumeanzisha vitalu vya miche ya miti kwa ajili ya upandaji katika maeneo yetu, sambamba na kutoa elimu ya mazingira mashuleni na kwa jamii. Tunawashukuru NEMC na Airtel kwa kushirikiana nasi na tunaomba ziara kama hizi ziwe endelevu,” alisema Bi. Vionatis.

Kampeni ya Pamoja Tutokomeze Taka za Plastiki inalenga kuelimisha jamii kuhusu athari za taka za plastiki na kuchochea ushiriki wa pamoja katika kuyafanya mazingira kuwa safi, salama na endelevu kwa vizazi vijavyo.

Powered by Blogger.