WANANCHI KUNUFAIKA NA MRADI WA KUZUIA BIASHARA HARAM
Na Saidi Lufune - Dodoma
Wananchi wa Kijiji cha Mlazo na Ndogowe wilayani Chamwino Jijini Dodoma wanatarajiwa kunufaika na Mradi wa kuzuia na kupambana na biashara haram ya ujangili (IWT) ili kujenga mahusiano mazuri dhidi ya Wanyamapori na kukuza sekta ya utalii nchini
Hayo yamesemwa leo Desemba 07, 2024 Jijini Dodoma na Afisa Wanyamapori Mkuu Bi. Rose Mdendemi wa Idara ya Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii katika Mafunzo ya kuwajengea uelewa wa pamoja wajumbe wa mradi huo wenye dhana ya kushirikisha jamii katika uhifadhi Wanyamapori kupitia Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori
Amesema lengo kuu la kushirikisha jamii katika uhifadhi ni kutekeleza sera ya Taifa ya Wanyamapori ya Mwaka 2007 inayohimiza Wananchi wanaoishi kwenye ardhi za vijiji vyenye rasilimali za wanyamapori na kuwajibika katika kuhifadhi rasilimali hizo.
“Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Halmashauri ya Wilaya Chamwino, Jimbo la Mvumi inaendelea na utekelezaji wa ushirikishaji jamii katika uhifadhi ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haram ya nyara. ” Amesema Bi. Rose
Katika hatua nyingine Bi. Rose amewataka askari Wanyamapori wa vijiji kufuata maadili ya kazi zao na kujenga mahusiano mazuri kati yao na jamii ili kuondoa uadui kati yao Wananchi na Wanyamapori
“Wizara itaendelea kuwawezesha kwa kuwapatia vitendea kazi kama mahema, pikipiki, kamera na kompyuta, kwahyo endeleeni kufanyakazi kwa ushirikiano na jamii kuhifadhi rasilimali za Wanyamapori ili ziendelee kutusaidia kupitia mradi huu” Amesema Bi. Rose
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Nghambaku Mhe. Harun Siengo ameishukuru Wizara ya Maliasili na utalii kupitia mradi huo kwa kuwa utasaidia wananchi kutumia fursa zitakazopatikana kujikwamua kiuchumi na kijamii ikiwemo kupata ajira, kujengewa hospitali na barabara
“Mradi huu utakua chachu ya maendeleo kwa wananchi lakini pia kujenga urafiki dhidi ya Wanyamapori kama Tembo, swala na Wanyama wengine kama walivyoweza kunufaika wananchi wa vijiji vingine tulivyovitembelea” Amesema Mhe. Siengo
Naye Afisa Maliasili na Mazingira wa Wilaya ya Chamwino Bi.Yustina Amo ametoa pongezi kwa wajumbe wa waliohudhuria Mafunzo hayo na kukubali Mradi huo kwakua itakwenda kuondo migogoro kati ya Maafisa wanyamapori jamii za ufugaji na wakulima kwa kujenga urafiki na kukuza shughuli za kutalii katika wilaya hiyo
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa vijiji hivyo wameipongeza serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutatua migogoro ya wanyamapori na wananchi wa maeneo hayo na kulipwa fidia kwa familia zilizoathiriwa na Tembo katika siku za hivi karibuni
Takribani shilingi billion tatu za kitanzania zimetolewa katika vijiji 230 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia faida zilizotokana na Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori ikiwa ni jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipa kipaumbele sekta ya utalii kwa kuutangaza utalii na kushirikisha na kukaribisha wafadhili
Post a Comment