NBS YA THIBITISHA WALIOJIANDIKISHA KUPIGA KURA
Na Jumanne Magazi
28.10.2024
Dar es salaam
Hatimaye Ofisi ya Taifa ya Takwimu Nchini (NBS) imesema taarifa iliyotolewa na serikali ya idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, ni sahihi na ni takwimu za serikali.
Kauli hiyo imekuja ikiwa zimepita siku chache, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa kutoa taarifa juu ya matokeo ya zoezi la uandikishaji wapiga kura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 zilizotumika katika uandikishaji wa orofha ya wapigakura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mapema mwaka huu.
“Taarifa hiyo ya Serikali ilionesha kuwa, wananchi waliojiandikisha kushiriki katika uchaguzi huo ni 31,282,331 sawa na asilimia 94.83 ya watu wote wenye umri wa kujiandikisha kwa mwaka 2024.
“Hata hivyo, tangu kutolewa kwa taarifa hiyo, kumekuwepo na taarifa za kupotosha takwimu hizo kwenye baadhi ya vyombo vya habari hususan mitandao ya kijamii kwamba takwimu za wananchi walioandikishwa hazina uhalisia na kwamba idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya watu wanaostahili kujiandikisha kupiga kura inayotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022,” alisema.
Dk. Albina alisema takwimu wanazozizungumzia watu hao ni takwimu zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na kwamba ulinganishaji wanaoufanya hauendani na hali halisi ya idadi ya watu wenye sifa za kujiandikisha kupiga kura mwaka huu.
Alisema kwa hesabu za kawaida idadi ya watu nchini kwa mwaka 2022 haiwezi kulingana na idadi ya watu kwa mwaka 2024 kwani hivi sasa tayari miaka miwili kamili imeshapita tangu ikufanyika kwa sensa hiyo.
“Kutokana na makadirio ya idadi ya watu kwa 2024, idadi ya watu nchini inakadiriwa kuwa Milioni 66.3 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 3.2 kwa mwaka kama ilivyopatikana kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
“Makadirio haya kwa Tanzania Bara yanakadiriwa kufikia watu milioni 64.2 na kwa Tanzania Zanzibar yanakadiriwa kufikia watu milioni 2.03, kwa makadirio haya, wananchi tunapaswa kufahamu kuwa idadi ya watu kwa mwaka 2024 haiwezi kuwa sawasawa na ile ya mwaka 2022,” alisema.
Alifafanua kuwa watu waliokuwa na umri wa miaka 16, 17 na 18 katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 hivi sasa wana umri wa miaka 18, 19 na 20 ambao idadi yao ni 3,785,036 waliokidhi kigezo cha umri wa kujiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka huu.
Pamoja na mambo mengine amesema ni wakati sasa nchini kushirikiana na Kuunga mkono jitiahada za mh Rais ili kuhakikisha Taifa linafikia maendeleo iliyojiwekea
Post a Comment